KATIKA miongo kadhaa iliyopita filam nyingi zenye mafanikio zimetokezwa huko Hollywood. Hilo limekuwa na uvutano mkubwa ulimwenguni pote kwani filam nyingi za Marekani hutazamwa katika nchi nyingine majuma machache au hata siku chache tu baada ya kuonyeshwa kwa mara ya kwanza nchini Marekani. filam fulani hata zimeonyeshwa kwa mara ya kwanza tarehe ileile duniani kote. Dan Fellman, rais wa usambazaji wa filamu nchini Marekani wa shirika la Warner Brothers anasema hivi: “Soko la ulimwenguni kote la uuzaji wa filam linazidi kukua nalo linasisimua sana, kwa hiyo tunapotengeneza filam, huwa tunaitengeneza kwa ajili ya soko la ulimwenguni kote.” Sasa kuliko wakati mwingine wowote, kile kinachotendeka huko Hollywood huathiri biashara ya filam ulimwenguni
Lakini kupata faida kutokana na filam si rahisi kama unavyowazia. filam nyingi zinahitaji zaidi ya dola milioni 100 ili kulipia gharama ya kuzitengeneza na kuziuza. Na kufanikiwa kwake kunategemea watazamaji ambao mtu hawezi kutabiri watapendezwa na nini. David Cook, profesa wa masomo ya filam katika Chuo Kikuu cha Emory anasema hivi: “Huwezi kujua ni lini jambo fulani litawavutia au kuwasisimua watazamaji.” Kwa hiyo watengenezaji wa filam huongezaje uwezekano wa filam yao kufanikiwa? Ili kupata jibu, tunahitaji kuelewa mambo machache ya msingi yanayohusika katika utengenezaji wa filam.*