Kupiga picha za sinema kunaweza kuchukua wakati mwingi, kunaweza kuchosha, na pia kunaweza kugharimu pesa nyingi. Kwa kweli, kupoteza dakika moja tu kunaweza kugharimu maelfu ya dola. Nyakati nyingine inabidi waigizaji, wafanyakazi, na vifaa visafirishwe hadi sehemu ya mbali. Hata hivyo, haidhuru picha hizo zitapigiwa wapi, lazima pesa nyingi sana zitatumika kila siku.
Watu wanaoshughulikia mwangaza, wale watakaowapamba na kuwatengeneza nywele waigizaji huwa kati ya watu wa kwanza kufika mahali ambapo picha zitapigiwa. Kila siku ya kupiga picha, waigizaji wakuu hupambwa kwa saa kadhaa. Kisha picha hupigwa kwa siku nzima.
Mwelekezi husimamia kwa uangalifu kupigwa picha kwa kila onyesho. Inaweza kuchukua siku nzima kupiga picha za onyesho fupi sana. Picha za maonyesho mengi katika sinema hupigwa kwa kutumia kamera moja, kwa hiyo, onyesho moja linaweza kupigwa picha kadhaa kutoka pembe tofauti-tofauti. Isitoshe, huenda onyesho lilelile likapigwa picha mara kadhaa ili kupata picha bora zaidi au kurekebisha tatizo la kiufundi. Ikiwa onyesho ni refu, huenda picha 50 au zaidi zikapigwa! Kwa kawaida, mwishoni mwa kila siku, mwelekezi huchunguza picha zote na kuamua ni zipi zitakazotumiwa. Kazi ya kupiga picha inaweza kuchukua majuma au hata miezi kadhaa.
Katika hatua hii, picha zilizopigwa huboreshwa na kupangwa zinavyopaswa kufuatana. Kwanza, muziki utakaotumiwa huambatanishwa na sinema hiyo. Kisha, mhariri huunganisha sehemu za sinema hiyo na kufanyiza nakala ya kwanza isiyo kamili.
Madoido ya sauti na picha pia huongezwa katika hatua hiyo. Nyakati nyingine kompyuta hutumiwa kutia madoido hayo katika hatua hii ambayo ni mojawapo ya sehemu ngumu zaidi za utengenezaji wa filamu. Kazi inayofanywa katika hatua hii inaweza kuifanya sinema ivutie na ionekane kuwa halisi.
Muziki uliotungwa hasa kwa ajili ya sinema hiyo huongezwa katika hatua hiyo, na jambo hilo ni muhimu katika filamu za leo. Edwin Black anaandika hivi katika gazeti Film Score Monthly: “Sasa watengenezaji wa sinema hutaka muziki uliotungwa hasa kwa ajili ya sinema, nao hawataki muziki wa dakika ishirini tu au vipindi vifupi vya muziki, bali wao hutaka muziki utakaochezwa kwa muda unaozidi saa nzima.”
Nyakati nyingine filamu iliyoboreshwa huonyeshwa watu wachache ambao wanaweza kutia ndani rafiki za mwelekezi au wafanyakazi wenzake ambao hawakuhusika katika kutengeneza filamu hiyo. Ikitegemea jinsi watakavyoitikia, mwelekezi anaweza kupiga picha upya maonyesho fulani au kuyaondoa kabisa. Katika visa fulani, umalizio wote wa filamu ulibadilishwa kwa sababu watu walioitazama kwanza hawakuupenda.
Hatimaye, filamu iliyokamilika huonyeshwa kwenye majumba ya sinema. Ni wakati huo tu ndipo inaweza kujulikana ikiwa sinema hiyo itafanikiwa au haitafanikiwa, au itakuwa ya wastani. Lakini mambo mengi yanahusika kuliko kupata faida. Sinema kadhaa zikikosa kufanikiwa zinaweza kuharibu sifa ya mwelekezi na matarajio ya mwigizaji kupata kazi. Anapofikiria miaka yake ya mapema ya kutengeneza filamu, mwelekezi John Boorman anasema hivi: “Niliwaona waelekezi wenzangu wakikosa kandarasi baada ya sinema kadhaa walizoelekeza kukosa kufanikiwa. Ukweli wenye kusikitisha ni kwamba katika biashara ya kutengeneza sinema, usipowaletea faida mabwana zako, unapoteza kazi yako.”
Bila shaka, watu wanapotazama ubao wa kutangazia sinema, kwa ujumla hawafikirii ikiwa watengenezaji wa sinema hiyo watapoteza kazi zao au la. Yaelekea wao huhangaikia mambo kama: ‘Je, nitafurahia sinema hii? Je, inafaa nitumie pesa zangu ili kuitazama? Je, sinema hii itanivutia au itanichukiza? Je, inawafaa watoto wangu?’ Unaweza kujibuje maswali hayo unapoamua sinema utakazotazama?