Mara nyingi, matayarisho yanayofanywa kabla ya upigaji picha ndiyo sehemu muhimu zaidi ambayo huchukua muda mrefu katika utengenezaji wa sinema. Kama tu ilivyo na mradi wowote mkubwa, mafanikio yake hutegemea sana matayarisho. Inatumainiwa kwamba pesa zozote zinazotumiwa wakati wa matayarisho zitapunguza sana gharama za kutengeneza filam yenyewe.
Kutengenezwa kwa filam huanza na hadithi fulani ambayo huenda ikabuniwa au ikategemea matukio halisi. Mwandikaji huandika hadithi hiyo kwenye hati. Hati hiyo inaweza kufanyiwa marekebisho mengi kabla ya hati ya mwisho kutokezwa. Hati hiyo ya mwisho huwa na wahusika pamoja na maelezo mafupi kuhusu kitendo kitakachofanywa. Pia hati hiyo hutoa maagizo mengine kama vile mahali ambapo kamera zitakuwa na mabadiliko yatakayofanywa katika kila onyesho.
Hata hivyo, hati hiyo inapokuwa katika hatua za kwanza, mtayarishaji atakayeinunua huanza kutafutwa.* Mtayarishaji anaweza kupendezwa na hati ya aina gani? Kwa kawaida sinema ambayo hutolewa msimu wa kiangazi hukusudiwa iwavutie vijana wa kati ya miaka 13 hadi 25 hivi. Kwa hiyo mtayarishaji atapendezwa hasa na sinema ambayo itawavutia vijana.
Hati inayofaa hata zaidi ni ile itakayowavutia watu wa umri mbalimbali. Kwa mfano, bila shaka sinema inayotegemea shujaa anayetajwa katika vitabu vya vibonzo itawavutia watoto wadogo ambao wanamfahamu shujaa huyo. Na bila shaka wazazi wao wataambatana nao kuitazama sinema hiyo. Lakini watengenezaji wa sinema huwavutiaje vijana walio na umri wa kati ya miaka 13 na 25 hivi? Katika gazeti The Washington Post Magazine, Liza Mundy anasema kwamba “habari inayosisimua” ndiyo jambo muhimu. Ili sinema “ilete faida kubwa na kuwavutia watu wa umri mbalimbali bila kupuuza yeyote,” lugha chafu, jeuri nyingi, na picha nyingi za ngono hutiwa ndani..
Mtayarishaji akiona kwamba hati inaweza kuwa sinema nzuri, huenda akainunua na kumpa kandarasi mwelekezi na mwigizaji maarufu. Kuwa na mwelekezi na mwigizaji maarufu kutafanya sinema hiyo ivutie sana wakati itakapotolewa. Hata katika hatua hii ya kwanza, waelekezi na waigizaji maarufu wanaweza kuwavutia wawekezaji wanaohitajika ili kugharimia utayarishaji wa filam hiyo.
Hatua nyingine ya matayarisho ni kuchora vibonzo mbalimbali vya filamu hiyo hasa vile vinavyohusisha mapigano. Michoro hiyo humwongoza mpiga-picha za sinema nayo husaidia kupunguza wakati unaotumiwa kupiga picha. Mwelekezi aliye pia mwandikaji wa hati, Frank Darabont, anasema: “Hakuna jambo baya zaidi kama kupoteza wakati wa kupiga picha kwa sababu tu ya kutojua mahali ambapo kamera inapaswa kuwa.”
Kuna mambo mengine mengi muhimu yanayopaswa kushughulikiwa wakati wa matayarisho. Kwa mfano, picha zitapigiwa wapi? Je, itakuwa lazima kusafiri? Je, kuna picha zitakazopigwa ndani ya nyumba, nayo itapambwaje? Je, mavazi maalumu yatahitajika? Ni nani atakayeshughulikia mwangaza, kupamba na kutengeneza nywele za waigizaji? Na vipi kuhusu sauti, madoido, na yule atakayeigiza sehemu hatari badala ya mwigizaji mkuu? Hayo ni baadhi ya mambo yanayohitaji kufikiriwa hata kabla ya kupiga picha za filamu. Ukitazama majina yanayoonyeshwa mwishoni mwa sinema inayotazamiwa kuleta faida kubwa, huenda ukaona kwamba mamia ya watu walihusika kuitayarisha! Fundi mmoja wa mitambo ambaye amehusika katika kutengeneza sinema nyingi anasema kwamba “watu wengi sana huhusika katika kutengeneza filamu nzuri.”